Jambo TV's banner
Jambo TV's profile picture

Jambo TV

@Jambotv_ • 960,470 subscribers

Independent News Source | WhatsApp+255767252999

Videos

Jambotv_'s profile picture

VIDEO: Kauli ya Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Idara ya Oganaizesheni, Paul Chacha, kusema vyombo vya ulinzi na usalama na viongozi wa serikali ni mali ya CCM, akidai kuwa chama hicho ndicho kilichowaweka katika nafasi hizo, imeendelea kuibua mjadala nchini Tanzania. Wakati wa mjadala wa Utawala wa Sheria uliorushwa kupitia kipindi cha Medani Kuu cha Star TV chini ya mtangazaji Edwin Odemba (Chief Odemba) Jumamosi Oktoba 10, 2026, Wakili Leonald Manyama na Wakili Dickson Matata wamechambua kauli hiyo ambapo Manyama ameeleza kuwa vyombo vya ulinzi na usalama msingi wake ni mali ya wananchi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, lakini akasisitiza kuwa video ya kiongozi huyo wa CCM imesambazwa ikiwa imekatwa bila kuangalia muktadha halisi wa mazungumzo. "Vyombo vya ulinzi na usalama havipokei maagizo kutoka Chama cha Mapinduzi. Vinapokea maagizo kutoka kwa Amiri Jeshi Mkuu ambaye ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambaye amepewa mamlaka hayo na wananchi kwa kura zao... Anapotoa maagizo kwa vyombo vya ulinzi na usalama hawi kama Mwenyekiti wa CCM, anatoa kama Amiri Jeshi Mkuu." Ameeleza Manyama. Wakili Manyama ameongeza kuwa mawaziri wanaowasilisha bajeti za wizara za ulinzi na usalama bungeni wanatokana na CCM na wameteuliwa na Rais anayetokana na chama hicho, hivyo kutoa wajibu kwa CCM kuhakikisha vyombo hivyo ili kulinda taifa. Kwa upande wake, Wakili Matata amepinga vikali utetezi huo, akisema kuwa maelezo ya Manyama yanaakisi kilekile alichokisema Chacha kwamba CCM inavichukulia vyombo vya ulinzi na usalama ama mali yake ya chama. Matata amebainisha kuwa mtazamo huo unapingana wazi na Katiba inayotaka vyombo hivyo kubaki huru bila kuunganishwa na chama chochote cha siasa.

Jambo TV

36,563 views • 9 days ago

Jambotv_'s profile picture

VIDEO: Miaka minane baada ya kifo cha mfanyabiashara na mmiliki wa Kampuni ya Mabasi ya Super Sami, Josiah Methusela Mzuri(Super Sami) Mahakama ya Rufani ya Tanzania imefuta hukumu ya kifo iliyokuwa imewatia hatiani John Simon(Kadaso) na Paul Mashauri (Nchimika,Rubembeja, Jam Marshal) baada ya kubaini mapungufu katika ushahidi uliotumika kuwahukumu. Uamuzi huo umetolewa Septemba 21, 2026 katika shauri la jinai la rufani namba 432/2024 lililokuwa mbele ya jopo la watatu Majaji watatu Kente, Kihwelo na Masabo ambapo mahakama hiyo ilikubaliana na hoja za upande wa waombaji ukiongozwa na Wakili Peter Kibatala Peter Kibatala kuifuta hukumu ya Mahakama Kuu na waliokuwa washtakiwa wakiachiwa huru. Kifo cha Super Sami kilitikisa mwaka 2018, baada ya taarifa za kutoweka kwake kusambaa taarifa za vyombo vya habari za wakati huo zilieleza kuwa aliondoka Mwanza Februari 27, 2018 akielekea Simiyu kwa shughuli za biashara, lakini hakurejea nyumbani. Familia ilieleza kuwa kabla ya kutoweka, marehemu alimweleza mkewe kuwa angerudi akiwa na mgeni na baadaye, gari lake aina ya Nissan Patrol lenye namba T 323 BSF lilikutwa limeteketea kwa moto ndani ya Hifadhi ya Taifa ya Serengeti. Mahakama ya Rufani ilikataa matumizi ya dhana ya “last seen together” dhidi ya John Simon, ikisema haikuthibitishwa bila shaka kwamba alikuwa mtu wa mwisho kuwa na marehemu kabla ya kifo chake. Aidha, Mahakama iliona kuwa kulikuwa na mapungufu katika ushahidi wa gari, umiliki wake, tarehe ya mauaji na mlolongo wa ushahidi wa kimazingira. Kwa mtazamo wa Mahakama, katika kesi inayotegemea ushahidi wa kimazingira, kila kiungo muhimu lazima kiungane bila kuacha uwezekano mwingine wa kutokuwa na hatia. Hivyo Mahakama hiyo ilikubaliana na hoja za upande wa waombaji na kuruhusu rufaa hiyo huku hukumu ya hatia dhidi ya John Simon na Paul Mashauri ikifutwa, adhabu ya kunyongwa ikaondolewa na Mahakama ikaamuru waachiwe huru mara moja iwapo hawakuwa wanashikiliwa kwa sababu nyingine halali.

Jambo TV

86,826 views • 27 days ago

Jambotv_'s profile picture

VIDEO: Kaimu Kamanda wa Polisi wa Kanda Maalum ya Dar es Salaam, SACP Faustine Mafwele, ametoa taarifa leo katika ukumbi wa Central Police akieleza kuwa hali ya usalama jijini ni shwari kabisa na kila mwananchi anaendelea na shughuli zake bila kuingiliwa. Akizungumzia mchezo wa ligi kuu ya soka Tanzania Bara utakaofanyika Jumamosi tarehe 10 Oktoba 2026 majira ya jioni katika Uwanja wa Uhuru, Temeke, ambao utakutanisha timu za Simba na Yanga, Kamanda huyo amesema ulinzi na usalama umeimarishwa kwa kushirikiana na wadau wote. Aidha amewakumbusha mashabiki, wapenzi na wadau wote wa soka kujiepusha na vitendo vyote vinavyokwenda kinyume na sheria, kanuni za ligi na taratibu za mikusanyiko. Polisi imewataka timu zote mbili mchezo mzuri. Katika taarifa nyingine, polisi imethibitisha kupatikana kwa binti mmoja aitwaye Enjo Abayo, mwenye umri wa miaka 19, ambaye alidaiwa kutoweka na mtoto mdogo wa miezi 10 eneo la Kibada, Kigamboni. Katika uchunguzi, binti huyo alieleza kuwa aliondoka na mtoto huyo kwenda kumsalimia dada yake aliyepata ajali Kibaha baada ya waajiri wake kukataa kumruhusu. Polisi imewashukuru wananchi na wadau wa uchunguzi kwa kushirikiana ili tukio hilo litafutuliwe kwa muda mfupi. Aidha, SACP Mafwele amewahimiza wananchi kushiriki katika kampeni mpya iitwayo “Ongea na Kamanda” inayolenga kuwawezesha wananchi kuzungumza na makamanda katika ngazi mbalimbali ili kutoa changamoto za kiusalama na kupata suluhisho pale inapohitajika. “ukisikia Kamanda yuko eneo fulani, nenda pale uweze kupata taarifa na kutoa changamoto ili tusaidiane kutatua matatizo ya kiuhalifu,” amesema Kamanda huyo.

Jambo TV

29,766 views • 11 days ago

Jambotv_'s profile picture

VIDEO: Waziri Mkuu wa Tanzania Dkt. Mwigulu Nchemba, leo Jumapili, Oktoba 4, 2026, amesimikwa rasmi kuwa Kanoni Mlei (Lay Canon) wa Kanisa Anglikana Tanzania katika ibada iliyofanyika katika Kanisa Kuu Anglikana la Kristo Mfalme Chanika, Dayosisi ya Handeni, mkoani Tanga. Dkt. Mwigulu amesimikwa katika wadhifa huo katika Ibada ya Misa Takatifu ya kuwekwa wakfu kwa Kasisi Canon Charles Mika Lundu kuwa Askofu wa Dayosisi ya Handeni. Dkt. Mwigulu alishiriki ibada hiyo kwa niaba ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan. Waziri Mkuu alitunukiwa cheo cha Kanoni Mlei na Kanisa Anglikana Tanzania, chini ya Askofu Mkuu wa Kanisa hilo, Dkt. Maimbo Mndolwa, Juni 21, 2026, katika Harambee ya kukamilisha mradi wa jengo la Kitega Uchumi cha Kanisa Anglikana Tanzania iliyofanyika katika Kanisa Kuu la Roho Mtakatifu, Jimbo la Dodoma. Kanisa Anglikana Tanzania lilimtunuku Waziri Mkuu cheo hicho kwa kutambua mchango wake katika kuhamasisha na kufanikisha uchangishaji wa fedha kwa ajili ya miradi mbalimbali ya maendeleo na vitega uchumi vya Kanisa hilo, tangu alipokuwa akitumikia nyadhifa mbalimbali za Serikali na kijamii. Kutunukiwa cheo hicho na hatimaye kusimikwa rasmi leo katika ibada iliyoongozwa na Askofu Mkuu wa Kanisa Anglikana Tanzania, Dkt. Maimbo Mndolwa, kumemfanya Waziri Mkuu kuungana na viongozi wengine wa Serikali waliowahi kutunukiwa wadhifa huo, huku akiwa Kanoni Mlei wa kwanza kutoka nje ya dhehebu la Anglikana, kwa mujibu wa taarifa hiyo. Viongozi wengine waliowahi kutunukiwa cheo cha Kanoni Mlei (Lay Canon) ni pamoja na Spika Mstaafu, Hayati Job Yustino Ndugai; Jaji Mkuu Mstaafu, Hayati Augustino Steven Lawrence Ramadhani; na Profesa Palamagamba John Kabudi, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu). Wengine ni Baraka Leonard, Katibu wa Bunge, pamoja na Gerald Mweli, Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo. Kwa mujibu wa taratibu za Kanisa Anglikana, Kanoni Mlei ni cheo cha heshima katika Kanisa hilo, ambacho miongoni mwa majukumu yake ni kutoa ushauri na kuwa mlezi wa uongozi wa juu wa Kanisa.

Jambo TV

32,467 views • 15 days ago